John Huus
Kanisa la Moravian lilianzishwa rasmi mwaka 1457 na wafuasi wa vuguvugu la mfia dini (shahidi) John Hus. Kanisa la Moravian ni madhehebu ya Kiprotestanti yenye zaidi ya miaka mia tano ya historia. Jina lake rasmi lilipoanza lilikuwa ni ‘’Umoja wa Ndugu’’; lakini likaja kujulikana zaidi kama Kanisa la "Moravian" miaka mingi baadaye katika karne ya kumi na nane (18). Jina hili la Moravian ilikuwa kwa sababu waumini wake wengi walitoka jimbo la Moravia, ambalo sasa lipo katika Jamhuri ya Ucheki ( Czech). Kanisa la Moravian kwa muda mrefu limekuwa mstari wa mbele katika jumuiya ya Kiprotestanti ulimwenguni, na ni miongoni mwa watu wa mwanzo kuchapisha Biblia katika lugha ya wananchi wenyeji (yaani nje ya lugha ya kiyunani),
Kanisa hili lilikuwa la kwanza kuchapisha nyimbo za kitabuni kwa lugha za wananchi wenyeji. Pia kanisa hili lilikuwa la kwanza kuweka msisitizo wa kuelimisha wanawake na wanaume; na walikuwa waanzilishi wa vuguvugu la misheni (Uinjilisti) ya Kiprotestanti tangu mwaka 1732. Wamoravian wamekuwa mstari wa mbele katika kukuza Umoja wa Kikristo katika historia yao yote, na ni mmoja wa waanzilishi wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni ( WCC), na Umoja wa Kikristo Tanzania (CCT).
Kituo cha kwanza cha misheni cha Moravian Tanzania kilianzishwa Rungwe Kusini mwa Tanzania mwaka 1891. Kituo kingine upande wa Magharibi mwa Tanzania kilikabidhiwa kwa Bodi ya Moravian huko Herrnhut, Ujerumani, na Shirika la Wamisionari la London (LMS) mwaka 1897. Ni kutokana na matokeo ya kazi ya uinjilisti ya vituo hivi viwili, kanisa la Moravian lilienea katika maeneo ya kusini na na magharibi mwa Tanzania na nchi nzima, kila moja lilikuwa na jimbo lake.
Haja ya kuanzisha ushirikiano kati ya Jimbo la Kusini na Magharibi ilionekana tangu mwanzo wa kuanzishwa kwao. Wamisionari waanzilishi walikuwa wameanzisha mawasiliano mapema kuanzia 1899. Baadaye walianza kukutana na kubadilishana uzoefu na majimbo hayo mawili na wakaanzisha ushirikiano katika mambo mbalimbali.
Mnamo 1965 walikubaliana kuunda rasmi Bodi ya pamoja ili kujadili na kukubaliana juu ya mambo ya msingi kwa majimbo yote mawili. Mnamo 1968 majimbo haya mawili yaliamua kuanzisha kwa pamoja Chuo cha Theolojia cha Moravian ( MOTHECO) kwa ajili ya mafunzo ya wachungaji; na mwaka 2004 kilisajiliwa rasmi kama Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji ( TEKU).
Mwaka wa 1976 Jimbo la Kusini liligawanywa mara mbili na hivyo kuwa Jimbo la Kusini na Jimbo la Kusini Magharibi, na hali hiyo hiyo ilifanyika kwa jimbo la Magharibi mwaka 1986 na kuwa Jimbo la Magharibi na Jimbo la Rukwa. Tangu wakati huo, mpaka wakati huu Kanisa la Moravian nchini Tanzania lina majimbo nane (8) na Majimbo ya Misheni mawili (2).
Pamoja na kuundwa kwa majimbo hayo mapya haja ya kuanzisha Kanisa la Moravian Tanzania kama chombo cha kitaifa cha kuratibu na kuunganisha kazi hiyo ikawa kubwa zaidi. Chombo hiki kingeweza kusimamia kwa pamoja programu mbalimbali za majimbo na kuwakilisha majimbo ndani na nje ya nchi.
Mnamo tarehe 04 Agosti 1986, wajumbe kutoka majimbo manne ya Tanzania walikutana Sikonge na kuazimia kuanzisha rasmi Kanisa la Moravian Tanzania (KMT) kama chombo cha kuwaunganisha Wamoravian wote nchini Tanzania. Mnamo 23 Novemba 1986, KMT ilizinduliwa rasmi mwezi Aprili 1987 ilisajiliwa rasmi katika mamlaka za serikali ya Jamhuri ya Tanzania. KMT ilitambuliwa rasmi na Sinodi ya Umoja wa Ndugu (Unitas Fratrum) katika mkutano mkuu wake huko Antigua, West Indies mwaka 1988.
KMT inawakilisha majimbo mbele ya serikali, makanisa mengine, mashirika mbalimbali, na mashirika ya kiekumene. Zaidi ya yote, jukumu lake kuu ni kupitia majimbo ni kuhubiri Injili Takatifu ya Wokovu ndani na nje ya kanisa. KMT pia inasimamia taasisi zote zinazomilikiwa na majimbo kwa pamoja.
Pia linafanya programu mbalimbali za kiroho na za kijamii. Miongoni wa programu hizo ni pamoja na kutoa elimu kupitia taasisi zake, semina na warsha mbalimbali. Kutoa elimu ya theolojia, uuguzi na utabibu, ufamasia, Ufundi, Uinjilisti, pamoja na taaluma mbalimbali ili kuchochea maendeleo katika jamii ya Kitanzania pamoja na nchi jirani. Programu kuu za kanisa ziko katika eneo la mafunzo ya wachungaji na wainjilisti kwa ajili ya uinjilisti na umisionari.
Kanisa la Tanzania linakua na waumini wanaongezeka kwa kasi. Na kwa sasa kanisa la linatoa huduma katika mikoa yote ya Tanzania na nje ya mipaka ya nchi, katika nchi za DRC, Malawi, Zambia, Kenya, Burundi, Rwanda, Angola, Msumbiji na Uganda.
Wamoravian kwa muda mrefu wamezingatia kuishi kwa uaminifu na Umoja wa Kikristo. Kanisa la Moraviani linahubiri misingi ya imani katika Maandiko Matakatifu yaani Biblia, ambayo Wakristo wote wanashiriki kwa pamoja. Wamoravian wanahimizwa kuishi kwa imani yao kwa njia ya huduma kwa ukamilifu wa mtu, yaani katika kuzingatia mahitaji ya kiutu, ambayo ni Kiroho, Kiakili na Kimwili.